ODM yamtetea Raila wakati mivutano Azimio ikirindima

Martin Mwanje
2 Min Read
Gladys Wanga, Mwenyekiti wa ODM

Chama cha ODM kimesitisha kimya chake na kumtetea kiongozi wake Raila Odinga dhidi ya madai kwamba amekiongoza chama hicho kujiunga na serikali. 

Viongozi wanne wa ODM siku chache zilizopita waliteuliwa kuwa mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza katika hatua ambayo imekosolewa vikali na vyama tanzu vya muungano wa Azimio.

Wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, viongozi kadhaa wa Azimio wanashikilia kuwa Raila hawezi kuwa serikalini na wakati huohuo kusukuma gurudumu la upinzani.

“Mtu fulani katika Azimio anajaribu kutilia shaka dhamira ya Raila Odinga kuiwajibisha serikali. Msingi wa kutilia shaka huko ni ukweli kwamba maafisa wanne, maafisa wanne tu wa zamani wa chama hiki walijiunga na serikali ya Kenya Kwanza ili kuleta uthabiti nchini,” walisema viongozi wa ODM wakiongozwa na mwenyekiti mpya wa chama Gladys Wanga.

“Tunasisitiza kwamba ukweli unasalia kile ambacho kiongozi wa chama Raila Odinga alichosema awali. Hakuna makubaliano kati ya ODM na Kenya Kwanza yanayofanya pande hizo mbili kuwa washirika serikalini.”

Kulingana na Wanga, wanachama wa ODM walioteuliwa kuwa mawaziri serikalini walifanya hivyo kwa misingi ya kibinafsi wala si kwa kukiwakilisha chama.

Wanachama hao ni John Mbadi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika) na Hassan Joho aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Madini.

Wanga ambaye pia ni Gavana wa Homa Bay akionya kuwa ODM kamwe haitaruhusu viongozi fulani katika muungano wa Azimio kumtumia Raila kama kinga kukidhia mapungufu yao ya uongozi.

“Kama chama, ODM haitakubali majaribio yoyote endelevu ya kumtumia Raila Odinga kama kinga ya binadamu, jaribio lolote endelevu la kumshawishi kumuidhinisha mtu yeyote kwa wakati huu, au jaribio lolote endelevu la kumtumia kama kisingizio  cha mapungufu ya uongozi katika vyama tanzu vya Azimio.”

ODM imetema cheche wakati Raila akiimarisha juhudi zake za kusaka uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.

 

Share This Article