ODM yakataa juhudi za kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi

Martin Mwanje
2 Min Read

Chama cha ODM kimepinga vkali mswada unaolenga kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi kutoka miaka 5 hadi 7. 

Mswada Uliopendekezwa wa Marekebisho ya Katiba Namba 2 wa 2024 umetayarishwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei.

“Tungependa kuelezea mashaka yetu kwa kupinga kabisa Mswada Uliopendekezwa wa Marekebisho ya Katiba Namba 2 wa 2024 kwa ujumla,” alisema Oduor Ong’wen, Mkurugenzi Mkuu wa ODM katika taarifa.

“Hatua yetu ya kukataa mswada huo imejitkita kwenye ukiukaji wa kifungu 255 (1) cha katiba ya mwaka 2010 na ukiukaji wa  muundo wake wa msingi.”

Kulingana na ODM, katiba inahitaji marekebisho kama hayo kuidhinishwa na Wakenya kwanza kupitia kura ya maoni.

Chama hicho sasa kinatoa wito kwa Bunge la Seneti kuukatalia mbali mswada huo na kwa kufanya hivyo kudumisha kanuni za maongozi bora na utawala wa sheria.

Bunge la Seneti linajiandaa kuujadili mswada huo ambao umepingwa vikali na Wakenya wakiwemo viongozi wa kidini.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana hapa nchini, ACK Jackson Ole Sapit, ameonya dhidi ya kupitishwa kwa mswada huo na Seneti.

Sawia na ODM, Ole Sapit anasema mdahalo wa kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi waliochaguliwa unapaswa kushughulikiwa kupitia kura ya maoni.

Mswada huo unapendekeza kuongezwa hadi miaka saba muhula wa kuhudumu wa Rais, Maseneta, Wabunge na Wawakilishi Wadi kutoka muhula wa sasa wa miaka mitano.

 

Share This Article