Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga amesema kwamba mswada wa marekebisho ya sheria ya ugavi wa mapato wa mwaka 2024 umezua kutoelewana kati ya bunge la Taifa na bunge la Seneti.
Akihutubia wanahabari leo, kiongozi huyo wa upinzani alisema kwamba mgogoro unaoshuhudiwa ni hatua ya kunyakua mamlaka na shambulio la katiba ya Kenya ambayo wabunge wanataka kutekeleza.
Kulingana naye hatua hiyo pia ni usaliti wakikatili kwa watu wa Kenya na mabadiliko katika mfumo wa utawala.
Raila anahisi kwamba saa hizi, usimamizi na ufadhili wa magatuzi unafaa kuwa unaimarika zaidi na ambao unaweza kubashiriwa ikitizamiwa kwamba magatuzi yamekuwepo kwa zaidi ya mwongo mmoja.
“Ninawaomba wabunge wawe wawezeshi wa magatuzi na wakatae kushirikiana na wale ambao wamejitolea kuhujumu na kuua ugatuzi.” alisema Raila.
Mwaniaji huyo wa wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika alitaja majukumu ya wabunge kama yalivyo kwenye katiba ambayo ni uwakilishi, utungaji sheria na uangalizi.
Kutokana na hilo alisema kwamba utekelezaji wa mipango haujawahi kuwa na hautawahi kuwa jukumu la wabunge wa bunge la taifa akisema lingekuwa jukumu lao basi mgogoro mbaya wa uwajibikaji ungeshuhudiwa katika mfumo wa utawala nchini.
“Katiba imeunda viwango viwili vya serikali, serikali ya kitaifa na serikali 47 za magatuzi na kusema kwamba magatuzi yapatiwe mgao wa angalau asilimia 15 ya mapato ya serikali ya kitaifa.” alisema Raila.
Amewataka wabunge wa bunge la taifa waelewe wazi kwamba mgao wa mapato kwa magatuzi hauwezi kupunguzwa ila unaweza tu kuongezwa.
Mswada wa marekebisho ya sheria ya ugavi wa mapato wa mwaka 2024 umezua utata ambapo wabunge wa bunge la taifa wanapendekeza mgao kwa kaunti uwe bilioni 380 kutoka kiwango kilichowekwa cha bilioni 400 huku maseneta wakitaka mgao huo usalie ulivyo.