Nyumba zote kuunganishwa na umeme miaka minne ijayo, asema Kindiki

Naibu Rais amesema nyumba milioni 10.3 kati ya jumla ya nyumba milioni 15.6 nchini tayari zimeunganishwa na umeme.

Martin Mwanje
1 Min Read
Serikali ya Kenya Kwanza ina mipango ya kuunganisha nyumba zote na umeme kote nchini katika kipindi cha miaka minne ijayo. 
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema nyumba milioni 10.3 kati ya jumla ya nyumba milioni 15.6 nchini tayari zimeunganishwa na umeme.
Akizungumza leo Alhamisi wakati akikagua mradi wa umeme wa Kiaumbui katika kaunti ya Kirinyaga, Prof. Kindiki alisema kati ya nyumba 10.3 zilizounganishwa na umeme, nyumba milioni 1.4 ziliunganishwa kati ya mwaka 2023 na sasa.
Miradi ya kuunganisha nyumba na umeme inaendelea katika kaunti ya Kirinyaga huku serikali ikilenga kuunganisha nyumba  7,300 zaidi na umeme kwa gharama ya shilingi milioni 440.
Mradi wa umeme wa Kiaumbui unalenga kuunganisha nyumba 149, biashara na asasi za umma na umeme kwa gharama ya shilingi milioni 10.9.
Wakati wa ukaguzi huo, Naibu Rais aliandamana na Naibu Gavana wa Kirinyaga David Githanda, mbunge wa Gichugu Gichimu Githinji na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni miongoni mwa viongozi wengine. 
Share This Article