Mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa Ndindi Nyoro, amesema maoni ya wakenya yatazingatiwa kabla ya kuidhinishwa kwa mswada wa kifedha wa mwaka 2024/2025.
Akiongea leo Jumamosi katika chuo cha kiufundi cha anuai cha Okame, eneo bunge la Teso kusini kaunti ya Busia wakati wa hafla ya kuchangisha fedha za makundi ya wanawake, Nyoro aliwataka wakenya kutokuwa na wasiwasi kuhusu swala la mswada huo.
Aidha, mwenyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa Kiharu, alisema kuwa bajeti hiyo ya mwaka wa kifedha 2024-2025, italeta afueni kubwa kwa wakenya hasa katika sekta kilimo, elimu na kuangazia maswala ya umeme mashinani miongoni mwa faida zingine.
Kauli ya Nyoro iliungwa mkono na mbunge wa Teso Kusini Mary Emase, ambaye aliwarahi wakenya kutokuwa na wasiwasi kuhusu mswada huo wa kifedha ambao umenuia kuleta suluhu kwa wakenya hasa kutatua masaibu ya walimu wa JSS.
Wakati huo huo Emase alikashfu vikali hatua ya baadhi ya viongozi kutoka eneo la Mlimani nchini, kuanzisha mchakato wa kukosoa serikali na kuonyesha nia ya kujitenga na wakenya wengine kwa kile amekitaja kuwa kukuza ukabila hapa nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka Muungano wa kenya Kwanza, wakiongozwa na msaidizi wa Rais aruk kibet, mbunge wa Nambale Geoffrey Mulanya miongoni mwa viongozi wengine.