NTSA yaongeza muda wa kufanya kazi kuimarisha utoaji huduma

Tom Mathinji
1 Min Read
Nambari mpya za usajili wa Magari.

Halmashauri ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA,  imetangaza kuongezwa kwa muda wa kufanya kazi kwa lengo la kuharakisha utoaji wa nambari za usajili wa magari,  leseni za kuendesha gari na stakabadhi za kumiliki magari.

Kupitia kwa taarifa, halmashauri hiyo ilisema afisi zake zitafunguliwa saa moja na nusu asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni, kinyume na hapo awali ambapo afisi hizo zilifunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni.

“Kama sehemu ya kuimarisha utoaji wa huduma, halmashauri ya NTSA imeongeza muda wake wa kufanya kazi,” ilisema taarifa ya NTSA Ijumaa asubuhi.

NTSA imetoa wito kwa watu ambao wamepokea ujumbe wa kuchukua nambari za usajili wa magari, kufika katika afisi zao.

“Tunawasihi waliopokea ujumbe wa kuchukua nambari za usajili wa magari, kufika katika vituo vya NTSA walivyotambua hapo awali,” ilisema NTSA.

Mabadiliko hayo yanajiri kufuatia agizo la waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen, la kuharakisha uchapishaji wa leseni za kuendesha magari, stakabadhi za kumiliki magari na nambari za kidijitali za usajili wa magari.

Murkomen aliyasema hayo Ijumaa wiki jana alipozuru kituo cha halmashauri hiyo cha Likoni Jijini Nairobi kutathmini utendakazi wake.

TAGGED:
Share This Article