NTSA: Kampuni mbili za uchukuzi wa umma zapokonywa leseni

Tom Mathinji
1 Min Read

Leseni za Kampuni mbili za uchukuzi wa abiria zimefutiliwa mbali na halmashauri ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani -NTSA, kwa madai ya kukiuka sheria za trafiki.

Kupitia kwa taarifa, halmashauri ya NTSA ilisema kampuni ya Bungoma Line Safari ltd na Smart Highways Sacco ltd, zilikiuka sehemu ya tano a sheria za NTSA za mwaka 2014, kwa kushindwa kuzingatia mwendo kasi.

Kampuni hizo mbili sasa zimetakiwa kuwasilisha magari yao kwa ukaguzi na kuthibitishwa utendakazi wa vidhibiti mwendo vya magari yao.

Kampuni ya Bungoma line Safaris imetakiwa kuwasilisha magari 162 kwa ukaguzi, huku ile ya Smart highways Sacco ikitakiwa kuwasilisha magari 29.

NTSA ilisema madereva 14 wa kampuni ya Bungoma Line safaris na wawili wa kampun ya Smart Highways Sacco, watafanyiwa majaribio upya, kabla ya magari hayo kurejeshewa leseni za kuhudumu.

Maafisa wa polisi waliagizwa kukamata magari ya kampuni hizo mbili ambayo yatahudumu kinyume na marufuku hayo.

Share This Article