Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imekemea vikali tukio lililomhusisha raia wa kigeni aliyewashambulia kwa matusi maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Diani, kaunti ya Kwale.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotiwa saini na msemaji wa NPS, Muchiri Nyaga, tukio hilo lilitokea Oktoba 28, 2025, ambapo mtuhumiwa, Elwin Ter Horst ambaye ni raia wa Uholanzi, alitumia lugha ya matusi kudhalilisha maafisa hao walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kisheria.
Huduma hiyo ililaani vikali tabia hiyo, ikieleza kuwa ni ya kudhalilisha, isiyokubalika kabisa na ya fedheha, ikisisitiza kwamba mienendo kama hiyo haitavumiliwa. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
NPS ilipongeza maafisa waliohusika kwa ustahimilivu, utaalamu na utulivu wao licha ya uchokozi, ikisema mwenendo wao unadhihirisha mageuzi yanayoendelea katika huduma hiyo yanayolenga kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na heshima kwa haki za binadamu.
Ikithibitisha tena kujitolea kwake kudumisha sheria na utulivu, NPS ilionya kwamba aina yoyote ya shambulio dhidi ya maafisa wa polisi ni kuvunja utawala wa sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa.
Huduma hiyo ilitoa wito kwa umma kushirikiana na maafisa wa polisi na kutumia njia rasmi za kuwasilisha malalamiko, ikisisitiza kuwa heshima ya pande zote kati ya polisi na wananchi ni nguzo muhimu ya amani na usalama.
Video iliyosambaa mitandaoni ya tukio hilo inamwonyesha mtuhumiwa, aliyetiwa mbaroni kwa kumshambulia mpenzi wake raia wa Kenya, akiwamiminia matusi maafisa wa polisi.
