Njuri Ncheke yaonya dhidi ya kuingia upinzani

Wanasiasa fulani wa Meru wanadaiwa kutishia kujiunga na upinzani iwapo mahakama haitadumisha kuondolewa kwa Gavana Mwangaza.

Marion Bosire
2 Min Read

Baadhi ya wanachama wa baraza la wazee la jamii ya Meru Njuri Ncheke na viongozi wa kaunti ya Tharaka Nithi, wameonya viongozi fulani wa kaunti ya Meru dhidi ya kuingiza watu wa kaunti hiyo kwenye upande wa upinzani.

Wakizungumza katika eneo la maabadi ya Njuri Ncheke huko Tigania Magharibi katika kaunti ya Meru, wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti Adriano Yaroyaro, walisema kuna mpango wa wanasiasa fulani wa kuingia upinzani.

Kulingana nao, mpango huo unategemea uamuzi wa mahakama katika kesi ya kuondolewa afisini kwa Gavana Kawira Mwangaza. Iwapo mahakama itakosa kumwondoa mamlakani Machi 14, viongozi hao wanapanga kujiunga na upinzani.

Wazee wa jamii ya Meru wanahisi kwamba hatua kama hiyo ni ya ubinafsi na inalenga kuharibu kabisa gatuzi la Meru lisiwahi kupata maendeleo.

Walisema wao kama wazee wa jamii, wanaunga mkono serikali ya sasa na wanamuunga mkono kikamilifu Rais William Ruto, naibu wake Kithure Kindiki na Gavana Kawira Mwangaza.

Wameapa kutolegeza kamba katika kuhakikisha jamii ya Meru haiingizwi kwenye upande wa upinzani.

Haya yanajiri baada ya baadhi ya wanasiasa wa kaunti ya Meru kuandaa mkutano Jumanne baada ya ule wa naibu Rais wa maendeleo na viongozi wa jamii na wa kisiasa katika makazi yake mtaani Karen jijini Nairobi.

Mkutano huo wa usiku unadaiwa kuwa wa kuafikia mambo watakayoitisha serikali na iwapo hawatayapata basi watajiunga na mrengo wa upinzani unaoongozwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *