Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance, UDA Cloephas Malala sasa amejitokeza kimasomaso na madai ya sababu iliyochangia kupigwa teke.
Malala amesema alifurushwa baada ya kupinga njama ya kutaka kumng’atua Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Akiwahatubia wanahabari siku ya Alhamisi, Malala alisema alipinga vikali hoja hiyo ya baadhi ya wanachama wa UDA wanaotaka Gachagua kutimuliwa kwa sababu za kibinafsi.
Aidha, Malala ameongeza kuwa wanaopanga njama hiyo wanataka kujiinua kisiasa ifikiapo mwaka 2027.
Seneta huyo wa zamani wa Kakamega tayari amewasilisha kesi kwenye jopo la kutatua migogoro ya vyama vya kisiasa kupinga kufurushwa kwake.
Gachagua alikashifu vikali jinsi Malala alivyotimuliwa ofisini na wadhifa wake kukabidhiwa aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar.