Nigeria, Cape Verde na Mali wamejikatia tiketi ya kushiriki makala ya 34 ya dimba la kombe la mataifa ya Afrika AFCON mwakani nchini Ivory Coast.
Super Eagles walifuzu Jumapili usiku baada ya kusajili ushindi wa mabao 3-2 ugenini Sierra Leone katika kundi A ,Victor Osihmen akibusu nyavu mara mbili kwa Nigeria.
Mali, maarufu kama Flying Eagles, walitinga kipute cha mwakani baada ya kupata ushindi wa mabao 2 kwa bila ugenini dhidi ya Congo katika kundi G.
Blue Sharks ya Cape Verde waliwahi tiketi baada ya kuigaragaza Burkina Faso magoli 3-1 katika kundi B na kuzoa alama 10.
Mataifa 14 yamefuzu kwa kindumbwendumbwe hicho wakiwemo wenyeji Ivory Coast, mabingwa watetezi Senegal, Guinea Bissau, Equitorial Guinea,Zambia, Afrika Kusini, Mali, Burkina Faso, Nigeria, Cape Verde,Tunisia, Algeria, Morocco na Misri.
Makala ya 34 ya patashika ya AFCON yataandaliwa nchini Ivory Coast kati ya Januari 13 na Februari 11 mwakani.