Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger wamefunga anga ya nchi hiyo kwa muda usiojulikana baada ya kukataa kutii makataa ya nchi za Afrika Magharibi ya kumrejesha mamlakani Rais Mohamed Bazoum au wakabiliwe kijeshi.
Tangazo hilo la jana Jumapili jioni lilijiri wakati ambapo wananchi wanaounga mkono mapinduzi walikusanyika kwenye uwanja wa michezo katika jiji kuu la Niger, Niamey kushangilia wanajeshi waliotekeleza mapinduzi, kundi ambalo linajiita “National Council for the Safeguard of the Homeland – CNSP”.
Msemaji wa kundi hilo la CNSP Amadou Abdramane, alitaja tishio la kukabiliwa kijeshi kutoka kwa umoja wa ECOWAS kuwa kichochezi cha hatua hiyo.
Kwenye taarifa iliyosomwa kupitia runinga ya taifa, Abdramane alisema wanajeshi walikuwa wakiandaliwa kwenye nchi mbili za Afrika ya Kati ili kushambulia walioongoza mapinduzi ila hakutoa habari zaidi.
Kulingana naye, wahudumu wote wa ulinzi wakisaidiwa na wananchi wa Niger wako tayari kulinda nchi hiyo.
Mapinduzi ya Niger yaliyotekelezwa Julai 26, 2023, ndiyo ya saba katika eneo la Magharibi na Kati mwa Afrika katika muda wa miaka mitatu sasa.
Eneo la Sahel linalokumbwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi ndilo limeshuhudia mapinduzi kama hayo.