Niger na Sudan zilifuzu kwa makala ya nane ya fainali za kuwania Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani maarifu CHAN mwaka ujao katika mataifa ya Kenya,Uganda na Tanzania.
Niger ilifuzu kwa sheria ya goli la ugenini baada ya kutoka sare tasa katika mechi ya marudio awamu ya mwisho jana dhidi ya wageni Togo,mechi iliyopigwa mjini Bamako,Mali.
Timu hizo zilikuwa zimeambulia sare ya bao moja katika mkumbo wa kwanza wiki jana mjini Lome Togo.
Niger watakuwa wakishiriki fainali za CHAN kwa mara ya tano
Awali Sudan ilikuwa timu ya kwanza kufuzu baada ya kuwalemea Ethiopia mabao 2-1 katika mechi ya marudio siku ya Jumatano.
Sudan maarufu kama Mamba wa Nile walifuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1, baada ya kuwapiga Wahabeshi 2-0 katika duru ya kwanza mjini Khartoum.
Timu 9 zitakazoshiriki kipute hicho zinatarajiwa kubainika Jumamosi,huku nne za mwisho zikijulikana Jumapili wakati wa mechi za mwisho za kufuzu.
Fainali za CHAN zitaandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Kenya,Uganda na Tanzania kati ya Februari mosi na 28.