Niger na Misri wasajili ushindi AFCON U-23

Dismas Otuke
1 Min Read

Niger na Misri walijiweka katika nafasi nzuri ya kutinga semi fainali ya kombe la mataifa ya Afrika kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 23 baada ya kupata ushindi wa bao moja kila moja katika mechi za kundi B raundi ya pili zilizopigwa Jumatano usiku ugani Ibn Batouta mjini Tangier, Morocco.

Katika mchuano wa kwanza, Misri waliishinda Mali bao 1 kwa bila, goli la ushindi likipachikwa kimiani na Mohammed Adel kunako dakika ya 10 na kudumu hadi kipenga cha mwisho.

Katika mchuano wa pili, Niger waliigutusha Gabon baada ya kuilaza kwa goli moja kwa sifuri.

Aboud Moumouni alifunga la ushindi kwa Niger kupitia penalti ya dakika ya 60 kufuatia kuangushwa kwa mshambulizi Abdoul Salam Boulhassane na beki Urie-Michel Mboula.

Niger na Misri wanaongoza kundi B kwa pointi 4 kila moja na wanahitaji sare katika mechi za mwisho, Niger wakimenyana na Mali nao Misri wakipambana na Gabon ili kufuzu kwa nusu fainali.

Abdoul Darankoum Moumouni wa Niger akisherehekea kufunga bao picha hisani ya Nour Akanja/BackpagePix

Timu tatu bora kwenye mashindano hayo zitafuzu kwa michezo ya Olimpiki jijini Paris nchini Ufaransa.

Website |  + posts
Share This Article