Naibu Rais Rigathi Gachagua atabaini leo Alhamisi ikiwa atasalia afisini au atafurushwa, wakati Bunge la Seneti litakapokamilisha kusikiza hoja maalum na kupiga kura kwa mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi yake.
Jana ilikuwa siku mahususi kwa Gachagua na mawakili wake kujitetea pamoja na mwasilishaji wa hoja hiyo ambaye ni mbunge wa Kibwezi Magharibi Eckomas Mwengi Mutuse kuhojiwa na mawakili wa mshatikiwa.
Naibu Rais alikanusha mashtaka yote 11 akisema hana hatia.
Katika ratiba ya leo, mawakili wanaoongozwa na Gavana James Orengo, wanaowakilisha upande wa mashtaka, watatoa ushahidi wao na pia kujibu maswali kutoka kwa Maseneta.
Huenda Maseneta wakalazimika kukesha bungeni iwapo watatoa uamuzi leo kutokana na muda mrefu unaotarajiwa kuchukuliwa kupiga kura kwa kila shtaka kumaanisha kuwa kila mmoja atapiga kura 11.
Baadaye, Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi atatangaza matokeo yatakayomwokoa au kumtema Gachagua kutoka afisini.
Ili kumbandua afisini Gachagua, Maseneta 45 wanapaswa kuunga mkono hoja hiyo huku mshatakiwa akihitaji kuungwa mkono na Maseneta 23 pekee kujinusuru.
Endapo ataenguliwa mamlakani, Gachagua atakuwa Naibu Rais wa kwanza kufurushwa afisini kupitia kura hiyo ya bunge.