Huenda pakachimbika Ijumaa usiku wakati miamba mabingwa watetezi wa AFCON, Senegal watakapokwangurana na Cameroon katika mchuano wa kundi C.
Indomitable Lions waliotoka sare na Guinea katika mechi ya ufunguzi wanahitaji kulazimisha sare ili kuwa na fursa ya kufuzu kwa raundi ya 16 bora.
Teranga Lions wa Senagal nao watalenga ushindi ili kuwa timu ya kwanza kuingia raundi ya pili baada ya kusajili ushindi wa magoli matatu kwa bila dhidi ya Gambia katika mchuano wa ufunguzi.
Pambano hilo litang’oa nanga saa mbili usiku Ijumaa kabla ya Gambia kumenyana na Guinea saa tano usiku katika mechi ya pili ya kundi C.
Itakuwa mara ya 9 kwa Cameroon na Senegal kupambana katika kipute cha AFCON, Simba wa Teranga wakishinda tatu, Simba wasiofugika wa Cameroon wakidedea mara mbili na mara tatu wakaishia sare.