Ngozi Ezeonu azomea wasichana waliovaa vibaya kwa majaribio ya kazi ya uigizaji

Mama huyo alionya kwamba yeyote atakayevaa vibaya katika majaribio anayohusika ataondolewa.

Marion Bosire
1 Min Read
Ngozi Ezeonu

Mwigizaji wa muda mrefu wa filamu za Nigeria Nollywood Mama Ngozi Ezeonu amegonga vichwa vya habari, kufuatia kusambaa kwa video inayomwonyesha akizomea wasichana fulani.

Ngozi alikuwa mmoja wa majaji wa majaribio ya kuigiza na hakufurahishwa na jinsi wasichana hao wa kizazi cha Gen Z walikuwa wamevaa.

Anaonekana kana kwamba anahutubia wengine waliokuwa wakisubiri zamu yao ya kujaribiwa ambapo alisema, iwapo yeyote atafika kwa majaribio kama hayo na mavazi sawa na mabinti hao basi angeondolewa mara moja.

Wasichana hao ambao amesimama nao wamevaa suruali ndefu za kunata mwilini, vishati tao visivyofunika vitovu na hawakuwa wamevaa sidiria.

Mama huyo alishangaa wawili hao walilenga kufurahisha nani kati ya majaji akiongeza kusema kwamba hata wakati alikuwa na umri kama wao, hangevutiwa na mavazi kama hayo.

Watumizi wengi wa mitandao nchini Nigeria na nje wametoa maoni yao kuhusu hatua ya Ngozi, wapo wanaomuunga mkono huku wengine wakimkashifu.

Wanaomuunga mkono wanasema majaribio ya uigizaji ni kama mahojiano ya kazi na hivyo mavazi ni muhimu huku wanaompinga wakisema wasichana hao walivaa kulingana na mitindo ya sasa.

Mama Ngozi Ezeonu ambaye sasa ana umri wa miaka 59, ameigiza tangu miaka ya 1990 na kabla ya hapo alikuwa mtangazaji wa runinga.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *