Ng’eno asema watarejesha pesa zilizofichwa ughaibuni

Marion Bosire
1 Min Read

Mbunge wa eneo la Emurua Dikir Johana Ng’eno amefichua kwamba serikali ina mipango ya kurejesha pesa ambazo ziliibwa na kufichwa ughaibuni.

Kulingana na mbunge huyo, matatizo ya sasa ya kiuchumi nchini Kenya yanatokana na wizi wa kiwango cha juu wa fedha za serikali uliofanyika chini ya serikali iliyopita.

Alisema shilingi trilioni 5 ziliibwa wakati huo.

Ng’eno aliambatanisha kupungua kwa thamani ya shilingi ya Kenya ikilinganishwa na dola na uhamishaji wa kiasi kikubwa cha fedha za nchi hii hadi nchi kama vile visiwa vya Cayman na Luxembourg.

Kiongozi huyo alisema atawasilisha bungeni mswada wa kuongoza mchakato mzima wa kurejesha fedha hizo.

Mswada huo utalazimisha kila mmoja kutangaza mali yake na wale ambao watakosa kutaja fedha ambazo wameficha ughaibuni watalazimishwa kuzirejesha nchini.

Anasema iwapo mpango huo utafanikiwa, pesa zitakazopatikana zinatosha kustawisha Kenya iweze kujitegemea kwa muda wa miaka miwili.

Share This Article