Wenyeji New Zealand wamewagutusha vigogo Norway baada ya kuwazabua Norway bao moja kwa bila katika mchuano wa ufunguzi wa kundi A wa makala ya 9 ya Kombe la Dunia kwa wanawake mapema Alhamisi.
New Zealand walianza mechi vyema wakitawala kipindi cha kwanza ingawa walikosa kumakinika mbele ya lango la Norway na kipindi cha kwanza kumalizika kwa suluhu bin sulushu.
Kipindi cha pili, wenyeji waliofurahia idadi kubwa ya mashabiki uwanjani walipachika bao la mapema kupitia kwa kiungo mkongwe Hannah Wilkinson, goli lililosambaratisha mchezo wa Norway.
New Zealand walipata penalti ya dakika ya 89 baada ya beki wa Norway kuunawa mpira lakini Ria Percival akagonga mlingoti.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa New Zealand katika historia ya Kombe la Dunia baada ya kucheza mechi 15 bila ushindi na wa kwanza baada ya miaka 32.
Fainali hizo za Kombe la Dunia zinashirikisha mataifa 32 kwa mara ya kwanza huku timu 9 zikifuzu kwa mara ya kwanza na zinaandaliwa kwa pamoja na Australia na New Zealand huku fainali ikisakatwa Agosti 20.