Netanyahu kuidhinisha kutwaliwa kwa Gaza

Netanyahu ataanzisha tena mazungumzo na Hamas ili kurejesha mateka wote waliobaki na kumaliza vita vilivyodumu karibu miaka miwili.

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema atatoa idhini ya mwisho ya kutwaa Jiji la Gaza huku akianzisha tena mazungumzo na Hamas yenye lengo la kurejesha mateka wote waliobaki na kumaliza vita vilivyodumu karibu miaka miwili, lakini kwa masharti yanayokubalika na Israel.

Akizungumza na wanajeshi karibu na Gaza Alhamisi, Netanyahu alisema bado anadhamiria kuidhinisha mipango ya kuteka Jiji la Gaza, kitovu chenye watu wengi katika Ukanda wa Palestina na kuwalazimisha karibu watu milioni moja kuhama huku akitekeleza uharibifu wa kimfumo wa nyumba za Wapalestina.

“Wakati huo huo nimetoa maagizo ya kuanza mara moja mazungumzo ya kuachilia mateka wetu wote na kumaliza vita kwa masharti yanayokubalika kwa Israel,” alisema Netanyahu na kuongeza “Tuko katika hatua ya kufanya maamuzi.”

Operesheni kubwa katika Jiji la Gaza inaweza kuanza ndani ya siku chache baada ya Netanyahu kutoa idhini ya mwisho katika mkutano na maafisa wa juu wa usalama baadaye Alhamisi.

Vikosi vya Israel tayari vimeongeza mashambulizi katika eneo hilo, na maelfu ya Wapalestina wameshakimbia makazi yao huku mizinga ya Israel ikizidi kusogea karibu na Jiji la Gaza katika kipindi cha siku 10 zilizopita.

Hamas ilisema mapema wiki hii kuwa imekubali pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na wapatanishi wa Qatar na Misri, ambalo, iwapo Israel itakubali, linaweza kuzuia mashambulizi zaidi.

Jeshi la Israel linapanga kuwaita tena wanajeshi wa akiba 60,000 na kuongeza muda wa huduma kwa wengine 20,000.

Pendekezo lililopo mezani ni ka kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuachiliwa kwa mateka 10 walioko hai wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza na miili ya watu 18.

Kwa upande wake, Israel itaachilia wafungwa wa Palestina wapatao 200.

Website |  + posts
Share This Article