Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezima uvumi ambao umekuwa ukienea kwamba ameaga dunia, kwa kuchapisha video fupi kwenye akaunti yake ya X.
Katika video hiyo, Netanyahu anaonekana akiwa kwenye mkahawa akiagiza kahawa huku akihojiwa na mtu ambaye alikuwa nyuma ya kamera.
Video iliyochapishwa awali ya Waziri huyo Mkuu wa Israel akitoa hotuba, ilikuwa na makosa kadhaa huku wadadisi wakiitaja kuwa iliyoundwa na akili unde na wala sio ya ukweli.
Video hiyo ilionyesha vidole vya Netanyahu kuwa zaidi ya vitano huku meno yake pia yakibadilikabadilika na kusababisha uvumi kuenea hata zaidi kwamba huenda aliuawa au kuumizwa vibaya katika mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel.
Katika ujumbe wake wa video jana Jumapili jioni, Netanyahu alihimiza raia wa Israel kutii maagizo ya usalama iwapo kutakuwa na mashambulizi ya roketi.
Alisema ustahimilivu wa watu wa Israel unatoa nguvu sio kwake tu bali pia kwa serikali, jeshi na kwa shirika la kijasusi la Mossad.
Netanyahu alisema kwamba kwa sasa, anajihusisha na mambo ambayo hawezi kuyataja lakini akakiri kwamba wanashambulia Iran na Lebanon vikali.
Jeshi la IRGC la Iran lilitishia Jumapili kumuua Netanyahu huku vita vilivyoanzishwa na Marekani kwa ushirikiano na Israel dhidi ya Iran vikiingia wiki ya tatu.