Kundi la Hamas linamnyoshea kidole cha lawama waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa ‘kuhujumu’ mpango wa kusitisha vita Gaza kwa kukosa kuhudhuria mazungumzo.
Serikali ya Israel haijatuma mwakilishi kwa mazungumzo ya kuwezesha kuanzishwa kwa awamu ya pili ya mpango huo iliyopangiwa kuanza Machi Mosi, 2025.
Mazungumzo kuhusu awamu za pili na tatu ya mpango huo yalistahili kufanyika katika wiki ya sita ya awamu ya kwanza.
Katika awamu ya kwanza, mateka wa vita vya Gaza wa pande zote mbili ambazo ni Palestina na Israel waliachiliwa huku wanajeshi wa Israel wakiondoka kwenye sehemu fulani za Gaza.
Usambazaji wa misaada pia ulirejelewa katika ukanda huo wa Gaza uliokumbwa na miezi 15 ya mashambulizi ya Israel.
Kulingana na makubaliano ya awamu hiyo ya kwanza iliyoanda kutekelezwa Januari 19, 2025, awamu ya pili ikikamilika, itapelekea kuachiliwa kwa mateka wote wa Israel na usitishaji kabisa wa mapigano.
Basem Naim, mmoja wa washirika wakuu wa afisi ya siasa ya Hamas anasema wanaamini serikali ya Israel imeanzisha michezo ya kuhujumu mpango huo na kuonyesha nia ya kurejelea mapigano.
Kulingana naye, kundi la Palestina linalotawala Gaza bado limejitolea kwa makubaliano ya kusitisha vita na limekuwa likitekeleza majukumu yake chini ya makubaliano hayo.
Naim analaumu Israel kukiuka baadhi ya kanuni za awamu ya kwanza ya mpango wa kusitisha vita kwani Wapalestina zaidi ya 100 waliuawa, misaada haikukubaliwa kikamilifu na kuahirishwa kwa kuondoka kwa wanajeshi kutoka kwa mapito ya Netzarim.
Mwanzo wa mwezi huu, maafisa wa Israel walithibitishia jarida ya New York Times kwamba madai ya Hamas dhidi ya Israel ya kukiuka mapatano ni ya kweli lakini serikali ya Israel imekanusha.
Kama sehemu ya mkataba wa kusitisha vita, Israel ilikuwa imekubali kuruhusu nyumba za muda elfu 60 na mahema elfu 200 kuingizwa Gaza lakini haikufanya hivyo.
Asilimia 90 ya wenyeji wa Gaza ambao ni milioni 2.4 walipoteza makazi na sehemu kubwa ya ukanda wa Gaza imesalia vifusi tu.
Israel imetekeleza mauaji ya Wapalestina elfu 48,319 tangu ilipoanzisha mashambulizi Gaza Oktoba 7, 2023. Afisi ya vyombo vya habari ya Gaza inaripoti kwamba watu elfu 13, hawajulikani waliko na wanachukuliwa kuwa walifariki.