Ndege zaidi za kukodi za Uingereza kutumwa Lebanon kuwahamisha raia wake

Martin Mwanje
2 Min Read

Uingereza itatuma ndege zaidi za kukodi kuwasaidia raia wake na wanaowategemea kuondoka nchini Lebanon.

Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imeyasema hayo leo Alhamisi wakati Israel ikiendelea kutekeleza mashambulizi makali mjini Beirut usiku kucha.

Raia zaidi ya 150 wa Uingereza na wanaowategemea walihamishwa kutoka mjini Beirut kwa ndege ya kukodi ya serikali ya Lebanon iliyowasili huko Birmingham, katikati mwa England, jana Jumatano, Wizara hiyo imesema.

“Idadi ndogo” ya ndege zitaondoka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rafic Hariri mjini Beirut Alhamisi, na “zitaendelea kufanya hivyo alimradi hali ya usalama inaruhusu.”

Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi John Healey kuitembelea Cyprus, ambako vikosi na wafanyakazi wa Uingereza wamepelekwa ili kujiandaa kwa uhamishaji wa watu unaoweza kufanywa.

Mashirika mengi ya biashara ya ndege yamesitisha safari kuelekea na kutoka mjini Beirut.

“Matukio ya hivi karibuni yameashiria hali inayoweza kubadilika nchini Lebanon”, alisema Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy jana Alhamisi.

Alisisitiza ujumbe wake wa kuwataka raia wa Uingereza “kuondoka nchini Lebanon mara moja”.

Hadi kufikia wiki jana, kulikuwa na raia wapatao 5,000 wa Uingereza na wanaowategemea nchini Lebanon, kulingana na makadirio ya serikali.

Israel imeongeza mashambulizi yake kusini mwa Lebanon na maeneo kadhaa ya mji wa Beirut, ikisema inalenga kuhakikisha usalama wa mpaka wake wa kaskazini baada ya karibu mwaka mmoja wa uhasama na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

Vita hivyo vimesababisha zaidi ya vifo 1,000 kufikia sasa.

Share This Article