Abiria 39 walinusurika baada ya ndege walimokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo ilipokuwa ikitua katika uwanja wa ndege wa Wilson.
Ndege hiyo kutoka Kisumu ilipoteza mwelekeo pindi tu ilipotua kwenye uwanja Ijumaa Jioni.
Kupitia kwa taarifa Halmashauri ya kusimamia viwanja vya ndege (KAA), imesema kisa hicho kilitokea mwendo wa saa 8:55 usiku.
“Tunathibitisha kuwa abiria wote 39 na wahudumu wa ndege hiyo wako salama bila majeraha…. shughuli za kawaida katika uwanja wa ndege wa Wilson zinaendelea kama kawaida” ilisema Halmashauri hiyo.
Ndege hiyo imesalia katika sehemu ya tukio katika uwanja huo huku uchunguzi ukiendelea.
Walioshuhudia walisema abiria walishuka upesi kutoka kwenye ndege hiyo pindi iliposimama huku maafisa wa uwanja wa ndege wakiwaongoza hadi sehemu salama.
Kiini cha ndege hiyo kukosa mwelekeo ilipotua bado hakijabainika.