Ndege iliyokumbwa na “msukosuko mkali” imetua kwa dharura nchini Brazil huku watu 30 wakiripotiwa kujeruhiwa.
Ndege ya Air Europa Boeing 787-9 Dreamliner ilikuwa ikisafiri kutoka Madrid kwenda Montevideo wakati tukio hilo la angani lilipotokea, shirika hilo la ndege lilisema.
Ndege ya UX045 ilielekezwa kwenye uwanja wa ndege wa Natal kaskazini mashariki mwa Brazil ikiwa njiani kuelekea mji mkuu wa Uruguay, kampuni hiyo ya Uhispania ilisema kwenye mtandao wa X, zamani ukijulikana kama Twitter.
Iliongeza kuwa abiria ambao walipata majeraha “wanapokea uangalizi”.
Ndege hiyo, iliyokuwa na abiria 325, ilikumbwa na msukosuko kwenye bahari ya Atlantiki ilipokuwa karibu kufika pwani ya Brazil, msemaji wa Air Europa alisema.
Ndege ilitua kama kawaida na ilikutana na kundi la ambulansi.
Maafisa wa uwanja wa ndege walisema baadhi ya abiria walihitaji usaidizi wa kimatibabu na walipelekwa katika hospitali ya karibu.
Timu ya madaktari wa eneo hilo iliambia vyombo vya habari vya Brazil kwamba walihudumia angalau abiria 30 wa mataifa mbalimbali na kwamba 10 kati yao walipelekwa hospitalini.
Wagonjwa hao walikuwa wamegonga vichwa vyao wakati wa msukosuko huo na kupata majeraha ikiwa ni pamoja na kuvunjika sehemu ya fuvu na majeraha usoni, timu hiyo iliongeza.
Tukio hilo linatokea wiki kadhaa baada ya ndege ya shirika la ndege la Singapore kukumbwa na msukosuko mkubwa nchini Myanmar, na kusababisha makumi ya majeruhi na kifo cha muingereza.
Msukosuko mkali ni nadra lakini tafiti za hivi karibuni zimeonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuongeza hatari ya hilo kutokea.