Ndege ya Kenya Airways yalazimishwa kutua Uingereza

Tom Mathinji
2 Min Read
Ndege ya shirika la Kenya Airways, yashurutishwa kutua Uingereza.

Ndege ya shirika la Kenya Airways iliyokuwa ikelekea katika uwanja wa kimataifa ya Hethrow Jijini London Uingereza,  ilielekezwa katika uwanja wa ndege wa Stansted, ikisindikizwa na ndege za kivita za Uingereza, katika hatua iliyotajwa kuwa tisho la usalama. 

Likithibitisha tukio hilo, shirika la ndege la Kenya Airways kupitia kwa taarifa siku ya Alhamisi, lilisema kuwa,” Kenya Airways plc (KQ) inathibitisha kwamba Alhamisi tarehe 12 Oktoba 2023, mwendo wa saa 10:30 BST, makao makuu yake yalipokea arifa kuhusu tishio la usalama kwenye ndege ya KQ100 iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi hadi London Heathrow. Usimamizi wa KQ kwa kushirikiana na mamlaka za usalama za Serikali ya Kenya na Uingereza zilifanya tathmini ya kina ya hatari ya tishio hilo,”.

Kulingana na msemaji wa wizara ya usalama  wa Uingereza, ndege za kivita za RAF Typhoon kutoka kitengo cha RAF Coningsby, zilitumika kama tahadhari kufuatilia ndege ya raia iliyokuwa ikikaribia Uingereza.

Msemaji huyo aliongeza kuwa, “Ndege hiyo ilisindikizwa hadi sehemu ya maegesho ya mbali na shughuli za kawaida za ndege zikiendelea,”.

Msemaji wa London Stansted alisema ndege ya Kenya Airways Boeing 787 “ilitua salama huku polisi wa Essex wakiihudumia”.

“Ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi hadi Heathrow ilielekezwa Stansted mchana huu. Uwanja wa ndege bado upo wazi.”

Ndege hiyo iko ardhini baada ya kutua Stansted, lakini polisi hawakusema ikiwa kulikuwa na tishio lolote linaloendelea, au ikiwa abiria walikuwa bado ndani.

Shirika la Kenya Airways, lilisema kuwa wafanyakazi waliokuwemo walipewa taarifa, na tahadhari zote za kiusalama zilichukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wetu na abiria waliokuwemo.

Share This Article