NCIC yakashifu shambulizi lililosababisha vifo vya watu wanane Marsabit

Tom Mathinji
1 Min Read
NCIC yakashifu shambulizi la Marsabit, ambapo watu wanane walifariki.

Tume ya mshikamano na utangamano wa taifa NCIC, imekashifu tukio ambapo watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki, walishambulia lori moja katika mpaka wa Kenya na Ethiopia na kusababisha vifo vya watu wanane.

Kulingana na Mamlaka, watu wengine wawili walijeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo, lililotokea katika barabara ya Eledimtu-Forole katika kaunti ya Marsabit.

Mwenyekiti wa tume ya NCIC  Samuel Kobia, alitaja tukio hilo kuwa hatari zaidi, ikizingatiwa eneo hilo limefurahia kipindi cha amani na utulivu katika muda wa miaka miwili iliyopita.

“Tumesikitishwa na shambulizi hilo, ambalo limesambaratisha amani iliyoshuhudiwa katika kipindi cha miaka miwili kupitia juhudi za NCIC,” alisema Kobia kupitia kwa taarifa.

Mwenyekiti huyo pia aliwapongeza viongozi wa eneo hilo ambao kwa pamoja walilaani shambulizi hilo.

Kobia alielezea wasiwasi kwamba shambulizi hilo la hivi punde huenda likasababisha ulipizaji kisasi kutoka kwa nchi jirani, akitoa wito kwa serikali kutumia rasilimali zilizopo kuzuia kisa sawia na hicho kutokea katika siku zijazo.

“Tunatoa wito kwa wakazi wa Marsabit kuwa watulivu huku asasi za serikali zikichunguza kisa hicho na kuwachukulia hatua waliohusika,” alisema Kobia.

Website |  + posts
Share This Article