Nchi zisizofungamana na upande wowote zatakiwa kuimarisha amani duniani

Tom Mathinji
3 Min Read
Rais wa Kenya William Ruto.

Rais William Ruto ameutaka Muungano wa nchi zisizofungamana na siasa za upande wowote (NAM), kutetea mageuzi yatakayoimarisha amani na usalama duniani, usawa wa mataifa na marekebisho ya usanifu wa fedha wa kimataifa.

Rais Ruto alitoa wito kwa muungano huo wenye nchi wanachama 120 kutoa mwongozo wa kimaadili ambao utahakikisha vyombo vya kimataifa na ahadi za kuweka chini silaha zinatekelezwa.

Hii, alielezea, itahakikisha Umoja wa Mataifa, mashirika ya kikanda yanatia juhudi zaidi kukuza amani, kuzuia migogoro, na kujenga amani.

“Enzi yetu inazidi kuwa na sifa ya kuongezeka kwa hatari ya migogoro ya silaha, kuenea tena kwa nyuklia, tishio la kuendelea kwa ugaidi, na itikadi kali kali, pamoja na changamoto zinazoibuka kama vile athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Rais alikariri kujitolea kwa NAM katika kulinda uhuru na mamlaka ya mataifa na kukuza uhuru kwa ukuaji jumuishi na endelevu.

Aliyasema hayo siku ya Ijumaa wakati wa Mkutano wa 19 wa Kilele wa NAM Jijini Kampala, Uganda.

Rais alizitaka nchi wanachama wa NAM kushinikiza kujumuishwa kwao katika mifumo ya kufanya maamuzi na usanifu wa kitaasisi wa usalama na utawala wa kimataifa na mfumo wa fedha wa kimataifa.

Alibainisha kuwa mfumo wa sasa si wa haki na ni rahisi kutumika na mataifa machache kunyanyasa mataifa mengine.

Kiongozi wa Nchi alisema kwamba mamlaka ya mataifa mengine yanatishwa wakati taasisi za kimataifa zinachukua hatua bila mashauriano, hatua zisizo na msingi, na mapendeleo katika utekelezaji wa sheria za kimataifa.

“Tangu kuanzishwa kwake, muungano wetu umekuwepo kulinda, kudumisha na kukuza maadili ya kudumu na ya kilimwengu ya uhuru, demokrasia na usawa wa mataifa ya ulimwengu,” alisema.

Rais Ruto alisema mageuzi katika usanifu wa fedha wa kimataifa yatahakikisha kuna mfumo wa kiuchumi wa haki na jumuishi ambao utakuwa na fursa sawa na jumuishi.

Alisema ipo haja ya kurekebisha mfumo uliopo aliouelezea kuwa wa kugandamiza, kutokubalika na kutokuwa endelevu akisema umeongeza mzozo wa madeni.

“Uungaji mkono wetu kwa ajenda hii utasaidia sana katika kupunguza kuongezeka kwa dhiki ya madeni katika nchi nyingi,” alisema.

Katika kikao cha ufunguzi wa mkutano huo unaoendelea mjini Kampala, Uganda, Rais Yoweri Museveni alichaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa NAM.

Uganda, ambayo inachukua nafasi hiyo kutoka kwa Azerbaijan, itahudumu kwa miaka mitatu katika Jukwaa hilo lililoanzishwa mwaka wa 1961.

Sudan Kusini inatarajiwa kuidhishwa kujiunga na NAM hii leo,Ijumaa.

TAGGED:
Share This Article