Namubiru aangazia uhusiano na mamake katika kitabu

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki maarufu wa Uganda Irene Namubiru, wiki hii amezindua kitabu chake cha kumbukumbu binafsi kinachofichua kwa undani uhusiano uliovunjika kati yake na mamake Justine Nyanzi Namawejje na familia yake.

Kitabu hicho kinaitwa “My Mother Knows: My Journey to Healing” na kilizinduliwa katika Hoteli ya Kampala Serena.

Kinaeleza kwa kina kuhusu uhusiano wake uliovunjika na wa mtafaruku na mama yake, hali ya kimya kati yao ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka kumi.

Irene anafichua jinsi uhusiano huo ulizidi kuwa mbaya baada ya tukio la kusikitisha mwaka 2013 nchini Japan, ambapo alisingiziwa makosa ya dawa za kulevya.

Badala ya kupata faraja kutoka kwa familia yake, alikumbana na kutojali na uhasama kutoka kwa mamake na ndugu zake, jambo aliloliona kama usaliti mkubwa uliosababisha kuvunjika kabisa kwa uhusiano wao.

“Kuandika kitabu hiki kwa hisia ni kama mzigo mzito umetoka mabegani mwangu” alisema akiongeza kwamba hakuficha habari hizo ili kumlinda mamake kwani alifahamu mengi aliyoyopitia, alijua, lakini alichagua kulinda watu waliokuwa wakimuumiza.

“Nilijikuta nikiwa nimefungwa kwenye mawazo ya kwamba, nikilalamika nitaonekana mbaya, na nikisema ukweli, watu hawataamini.” alisema msanii huyo.

Sababu ya mwisho iliyomsukuma Namubiru kuamua kuchapisha hadithi yake, ni mazungumzo ya simu aliyosikia kwa bahati mbaya.

“Wakati nilihisi nimechoka kumlinda mamangu, ni baada ya kumsikia akizungumza kwenye simu kuhusu mambo ambayo sikuweza kuamini,” alisimulia.

Mamake alikuwa anamweleza mgeni kwamba Irene anamchukia bibi yake na hatuwasaidii, jambo ambalo mwimbaji huyo alisema si la kweli.

La kutisha zaidi, mama yake alimshutumu kwa kufukua mabaki ya mababu zao kwa ajili ya uchawi.

“Hili liliogopesha sana, kwa sababu kufikia hapo walipiga simu polisi, na walinifanyia vurugu,” alikumbuka.

Website |  + posts
Share This Article