‘Nakuhitaji, nilikaribia kuwa mpweke serikalini,’ Ruto amwambia Kindiki

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto kwa mara ya kwanza ameelezea jinsi alivyokosa msaada wa Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua katika kueneza injili ya serikali. 

Amesema hali hiyo ilimfanya kujihisi mpweke wakati akijitwika jukumu la kuwaelezea Wakenya miradi inayotekelezwa na serikali yake.

“Prof. Kindiki mpendwa, nakuhitaji. Nahitaji weledi wako kunisaidia mimi na wanachama wa Baraza letu la Mawaziri kuelezea mambo tunayofanya, kuelezea vitu tunavyofanya,” alisema Rais Ruto wakati wa kuapishwa kwa Naibu wake mpya Prof. Kithure Kindiki.

“Nimekaribia kuwa mpweke katika serikali kuu hasa urais , nikizungumzia miradi yetu, nikizungumzia mipango yetu, nikifafanua juu ya kile tunachokifanya. Wewe ni mbuji, wewe ni mwerevu ndugu yangu. Nina imani kuwa utafanya kile ambacho nimekikosa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.”

Matamshi yake yakiashiria vuta ni kuvute iliyokuwepo kati yake na Gachagua katika kutekeleza Ajenda ya Mabadiliko ya serikali ya Kenya Kwanza ya kuanzia Chini hadi Juu (BETA).

Gachagua mara kadhaa alionekana kuwa na msimamo uliokinzana na ule wa Rais hususan kuhusiana na mipango kama vile uhamishaji wa watu kutoka maeneo yenye mito na makato ya nyumba.

Share This Article