Nakhumicha: Wizara ya Afya inakumbatia teknolojia kuimarisha utoaji huduma

Tom Mathinji
2 Min Read
Wizara ya Afyabyapokea vifaa vya kidijitali kutoka Shirika la Afya Duniani WHO.

Wizara ya afya imesema inaendelea kukumbatia utumizi wa teknolojia, ili kuimarisha utoaji huduma na kupanua huduma zake hadi katika maeneo ya mashinani.

Waziri wa afya Susan Nakhumicha, alisema kuwa mnamo mwezo Oktoba mwaka jana Rais William Ruto aliidhinisha sheria kuhusu huduma za afya kidijitali nambari 15 ya mwaka 2023.

Waziri huyo alisema kuwa sheria hiyo ambayo ilianza kutekelezwa mwezi Novemba mwaka jana, inawiana na mfumo wa kimataifa kuhusu utumizi wa dijitali katika sekta ya afya katika kuongeza operesheni na kuimarisha utoaji huduma za afya.

Akizungumza leo Ijumaa katika jumba la Afya Jijini Nairobi baada ya kupokea vifaa vya kidijitali kutoka shirika la Afya duniani WHO, Nakhumicha alisema serikali iko mbioni kufanikisha utoaji huduma za afya kwa wote UHC.

“Nashukuru WHO kwa msaada wa vifaa hivi vya kidijitali 940, ambavyo vitapiga jeki mipango ya kitaifa ya utoaji chanjo,” alisema Nakhumicha.

Aidha waziri huyo alisema kuwa serikali inajizatiti kusitisha vifo vya kina mama wajawazito wanapojifungua na watoto wanaozaliwa, huku ikihakikisha deta kuhusu chanjo inayonakiliwa ni sahihi.

Mwakilishi wa WHO nchini Kenya Dkt. Abdourahmane Diallo, alipongeza wizara ya afya kwa kutekeleza usimamizi wa deta kupitia njia ya kielektroniki maarufu  Chanjo-KE.

“Ili kuunga mkono hatua ya kukumbatia teknolojia, WHO imetoa vifaa vya kidijitali kutumika katika usimamizi wa deta, na itajumuisha chanjo zote ambazo zitatolewa,” alisema Diallo.

Share This Article