Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI kutoka kitengo cha kukabiliana na ugaidi kaunti ya Mandera, wamemkamata naibu wa chifu kwa kuhusika katika utayarishaji wa vitambulisho kwa raia wa kigeni kinyume cha sheria.
Yussuf Maalim Issak ambaye ni naibu wa chifu wa Bula Power mjini Mandera, alikamatwa kwa kujaribu kuwachukulia vitambulisho Isack Mohammed Abdi na Noor Yakub Ali, ambao ni raia wa kigeni wanaosakwa kwa madai ya kuwa magaidi.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema afisa huyo wa utawala anashukiwa kufanikisha upatikanaji wa hati ya usajili na kadi ya kusubiri kitambulisho kwa washukiwa hao wa ugaidi waliokamatwa walipokuwa wakipanga njama ya kuwateka nyara kundi la raia wa kigeni walioshiriki katika ujenzi wa bomba la taka mjini Mandera.
Makachero hao walisema maafisa wa usalama wanajitahidi kuhakikisha wakazi wa Mandera na viunga vyake wana usalama na amani.
“Hatua zimechukuliwa dhidi ya naibu huyo wa chifu, huku maafisa wa DCI na wale wa asasi zingine za usalama wakijizatiti kuhakikisha wakazi wa Mandera na viunga vyake wanaishi kwa amani wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku,” ilisema DCI kupitia ukurasa wake wa X.