Naibu Rais Rigathi Gachagua awataka viongozi wa dini kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa viongozi wa dini kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kupambana na tatizo la kusambaa kwa pombe haramu na dawa za kulevya nchini Kenya.

Akizungumza na viongozi wa dini katika makazi yake Karen, Gachagua aliwasihi “kuzungumza kwa ujasiri dhidi ya vitu hivi vinavyoletea watu kifo, kutoka kwenye madhabahu na katika hadhara zote.”

Wito huu unajiri baada ya janga la hivi karibuni huko Kiangai, Kaunti ya Kirinyaga, ambapo watu 17 walipoteza maisha baada ya kunywa pombe haramu.

Tukio hilo lilikuwa ukumbusho mkubwa wa athari mbaya za matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe katika jamii za Kenya.

“Kanisa lina nafasi muhimu kama sauti ya ushawishi na ushauri,” Gachagua alisema, akisisitiza uwezo wa viongozi wa dini wa kubadili maadili na tabia za kijamii.

“Sauti yenu inaweza kuwa chombo chenye nguvu katika kuongoza watu wetu kuelekea kwa maisha yenye afya na mafanikio zaidi.” aliongeza kiongozi huyo.

Alisisitiza haja ya mbinu mbalimbali katika kushughulikia suala hili gumu, zinazojumuisha hatua kali zaidi dhidi ya watengenezaji na wauzaji, pamoja na kampeni za uhamasisho wa umma na mipango ya kurekebisha tabia za wanaotumia dawa za kulevya.

Gachagua alisema Serikali haitaruhusu “Wafanyabiashara wa Kifo” kuendeleza biashara haramu ya pombe haramu, dawa za kulevya na vitu vingine wakati wa mkutano wa kushauriana na mawaziri Kindiki Kithure wa usalama wa ndani, Njuguna Ndung’u wa fedha, Susan Nakhumicha wa afya na mwanasheria mkuu Justin Muturi kuhusu kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya.

Ombi la Gachagua linalingana na juhudi zinazoendelea za mkewe, Dorcas Rigathi, ambaye amekuwa akitetea ustawi wa wavulana na vijana kwa bidii.

Kupitia taasisi yake, amekuwa akiongoza kampeni za kutokomeza matumizi mabaya ya dawa za kulevya na kukuza fursa za urekebishaji.

Bado haijulikani viongozi wa dini watajibu vipi wito wa Gachagua.

Hata hivyo, ushiriki wao unaweza kuwa muhimu katika kuhamasisha jamii na kukuza utamaduni unaozingatia afya na ustawi na kuepuka hatari za vitu haramu.

Share This Article