Naibu Rais Rigathi Gachagua awasili nchini Colombia

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua amewasili nchini Colombia anakotarajiwa kunadi kahawa ya Kenya na kuelezea mipango ya serikali ya kulainisha sekta hiyo humu nchini. 

Gachagua ametangaza kuwasili mjini Bogota akiwa ameandamana na ujumbe wake unaojumuisha wakulima wa zao hilo.

Ameahidi kufanya kila awezalo kulainisha sekta ya kahawa nchini kwa manufaa ya wakulima kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Akiwa nchini Colombia, Naibu Rais anatarajiwa kuhudhuria Kongamano la Wazalishaji na Wachomaji Kahawa Duniani litakaloandaliwa mjini Medellin.

“Mabadiliko ya sekta ya kahawa yanaendelea vizuri. Wakulima wetu lazima wanufaike na jasho lao kwa kuweka fedha zaidi mfukoni. Moja ya mikakati ya kufanya hivyo ni kuhusisha masoko yenye thamani ya juu ili kupata bei bora ya zao hilo,” alisema Gachagua punde baada ya kutua mjini Bogota.

“Itakuwa ziara yenye shughuli nyingi wakati pia tukishiriki makongamano ya ngazi ya juu ya kibiashara na mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wetu ambaye ni Makamu Rais, Francia Marquez.”

Colombia ni nchi inayoongoza katika uzalishaji wa kahawa duniani.

Inazalisha na kuuza kahawa katika mataifa kama vile Marekani, Ujerumani na Ubelgiji, mataifa ambayo Kenya inayalenga kupitia uongezaji wa thamani.

Colombia inazalisha takriban asiilimia 12 ya kahawa inayozalishwa duniani, na kuifanya kuwa nchi ya tatu katika uzalishaji wa kahawa duniani.

“Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwao. Pia tumesaini mkataba wa maelewano na Colombia, ambao utsaidia kuimarisha uhusiano uliopo wa pande mbili,” amesema Gachagua.

Baadaye, Gachagua atamwakilisha Rais Ruto kwa kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kundi la nchi zinazoendelea, G77 utakaoandaliwa nchini Cuba.

 

Website |  + posts
Share This Article