Naibu Rais Gachagua aandaa kikao na washirika wa maendeleo

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo ameandaa kikao na washirika wa maendeleo katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

Gachagua alisema kwamba Kenya imekuwa ikifurahikia uhusiano mwema na washirika wake wa maendeleo tangu ilipojipatia uhuru.

Kiongozi huyo aliongeza kwamba washirika hao wa kimaendeleo wametekeleza jukumu muhimu katika kusaidia Kenya kutatua changamoto kadhaa za kimaendeleo.

Lengo la mkutano wa leo kulingana na Naibu Rais ni kuimarisha mfumo faafu wa ushirikiano na kuhakikisha ushirika ambao utanufaisha wananchi wa Kenya na nchi kwa jumla.

Kikao hicho kilikuwa chini ya uenyekiti wake na balozi wa Uholanzi humu nchini Marteen Brouwer, na mshirikishi mkazi wa umoja wa mataifa Stephen Jackson.

Naibu Rais alitoa shukrani zake kwa washirika wa kimaendeleo akisema wamesaidia kujenga Kenya bora.

Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri na viongozi wengine wakuu serikalini.

Awali Naibu Rais alikuwa mwenyeji wa waziri wa masuala ya serikali na bunge nchini India Bwana Shri V. Muraleedharan katika makazi rasmi ya Karen.

Wawili hao hao walizungumzia masuala kadhaa kama vile ushirikiano wa kibiashara na ubadilishanaji wa ujuzi katika sekta za elimu, afya, Sayansi na Teknolojia, Utafiti, Utalii, Viwanda vya mazao ya kilimo, ujenzi wa nyumba na usimamizi wa benki.

Naibu Rais Gachagua na waziri Shri V. Muraleedharan
Share This Article