Naibu Gavana William Oduol: Kiti kugharimu shilingi milioni moja? Sikuhusika

Martin Mwanje
1 Min Read
Kiti kinachodaiwa kugharimu shilingi milioni 1 kinachosemekana kununuliwa na Naibu Gavana wa Siaya William Oduol.

Naibu Gavana wa Siaya William Oduol amekana kuhusika katika ununuzi wa kiti ambacho thamani yake inadaiwa kuwa shilingi milioni 1.12.

Kiti hicho kilizua msisimko miongoni mwa maseneta wakati wa kikao cha Kamati Maalum ya Seneti inayochunguza tuhuma dhidi yake kilichoandaliwa leo Alhamisi.

Kamati hiyo inaongozwa na Seneta William Kisang.

Oduol alikana madai ya kukiuka sheria za ununuzi kwa kulazimisha matumizi ambayo hayakuwekwa kwenye bajeti, hatua ambayo ilisababisha kutumiwa kwa shilingi zipatazo 18 kukarabati ofisi yake na shilingi milioni 1.12 kutumiwa katika ununuzi wa samani na vifaa vingine vya ofisi.

Awali, Oduol alikana tuhuma zote zilizowasilishwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na utumiaji mbaya wa wadhifa wake na ukiukaji wa katiba.

Hii ni baada ya Wawakilishi Wadi wote 42 wa bunge la kaunti ya Siaya kumtimua kufuatia mapendekezo ya jopo la wanachamana 14 lililobuniwa kumchunguza.

Wawakilishi Wadi wanamtuhumu kwa miongoni mwa mambo mengine kukiuka katiba na kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo.

Gavana James Orengo na Oduol ambaye ni naibu wake wamekuwa wakivurugana kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita huku Oduol akimnyoshea kidole cha lawama kwa kukimya wakati kukiwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *