Naendelea kuchapa kazi Ikulu, asema Rais Bio wa Sierra Leone

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio anasema anafanya kazi kwa bidii ya mchwa na kujitolea katika Ikulu ya nchi hiyo ili kutimiza vipaumbele vitano vikuu vya kitaifa vya nchi hiyo.

Lengo ni kufikia ukuaji endelevu wa jumla wa kiuchumi na maendeleo ya nchi hiyo.

Kauli zake zinawadia saa chache baada ya nchi hiyo kuweka amri ya kutotoka nje usiku baada ya watu waliokuwa na silaha kuwaachilia wafungwa kutoka gerezani.

Wafungwa kutoka magereza kadhaa makuu waliachiliwa huru jana Jumapili asubuhi, kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa nchi hiyo.

Serikali ya nchi hiyo imesema wengi wa waliohusika katika tukio hilo wamekamatwa, ingawa Rais Bio aliepuka kutaja kisa hicho kama jaribio la mapinduzi.

“Wajibu ulio mbele yetu ni mkubwa na wa dharura kiasi cha kutoweza kukawishwa na wale wanaotaufa kuvuruga amani na usalama tunaoufurahia kama nchi,” amesema Rais Bio katika taarifa aliyoipachika katika mtandao wa X.

“Kwa mara nyingine naelezea dhamira yangu ya kujenga Sierra Leone yenye amani na maendeleo inayofanya kazi kwa ajili ya wote.”

Share This Article