Pakistan imethibitisha kufanya mashambulizi katika miji ya Afghanistan ya Kabul na Kandahar, kulingana na afisa wa serikali, katika kile alichosema ni kulipiza kisasi.
Mashambulizi hayo yalitekelezwa saa chache baada ya Pakistan kusema wanajeshi wake wawili wameuawa kwenye operesheni ya Taliban wa Afghanistan kando ya mpaka.
Kulingana na Mosharraf Zaidi, msemaji wa waziri mkuu wa Pakistan, jumla ya Taliban 133 wa Afghanistan wameuawa na zaidi ya 200 wamejeruhiwa hadi sasa na vikosi vya Pakistan.
Lakini Zabihullah Mujahid, msemaji wa Taliban ya Afghanistan, aliandika kwenye X kwamba “hakuna mtu aliyejeruhiwa” katika mashambulizi hayo ya hivi karibuni ya Pakistan.
Wakati wa uhasama huu, pande zote mbili zimedai kusababisha hasara kubwa kwa upande mwingine huku zikipata uharibifu mdogo kwa upande wao.
Wizara ya ulinzi ya Taliban imesema iliteka vituo 19 vya kijeshi vya Pakistan na kambi mbili Alhamisi usiku na jumla ya wanajeshi 55 wa Pakistani waliuawa.
Huku hayo ykijiri, Iran imesema iko tayari kupatanisha nchi hizo mbili, kwa lengo la kumaliza mzozo huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa Iran iko tayari kuwezesha mazungumzo kati ya Pakistan na Afghanistan.
Kwenye taarifa aliyochapisha kwa mtandao wa X, Araqchi alisema: “Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni mwezi wa kujizuia na kuimarisha mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu, inafaa Afghanistan na Pakistan kushughulikia na kutatua tofauti zao za sasa kwa kuzingatia ujirani mwema na kupitia mazungumzo”.
Alisema Iran iko tayari kutoa kila aina ya msaada ili kuwezesha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha uelewano pamoja na ushirikiano.
Iran tayari ilikuwa imewahi kujitolea kupatanisha nchi hizo mbili hapo awali wakati mvutano wa mpakani ulipokuwa unaongezeka.