Mwili wa Marco Joseph Bukuru, mmoja wa waimbaji wa kundi la Zabron Singers ulizikwa jana Jumapili kwenye makaburi ya Nyakato, kata ya Nyasubi mjini Kahama nchini Tanzania.
Marco alikata roho Agosti 21, 2024 baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo katika hospitali kuu ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Jamaa huyo alipata matatizo ya moyo tarehe 10 Agosti, 2024 akiwa njiani pamoja na waimbaji wenzake kuelekea Kisumu nchini Kenya kwa ajili ya kambi za kanisa la kiadventista.
Marco alikuwa akiendesha gari lililokuwa limebeba waimbaji wa Zabron ghafla akaliegesha kando ya barabara akisema moyo unauma. Alifanyiwa huduma ya kwanza na wenzake kisha wakaendelea na safari.
Walifika Kisumu ambapo aliendelea kulalamikia maumivu ya moyo akapelekwa hospitalini jijini Kisumu ambapo madaktari walisema kwamba alikuwa amekumbwa na mshtuko wa moyo.
Baadaye, alirejea nyumbani Tanzania akatibiwa kwenye hospitali ya Bugando na kupatiwa rufaa hadi hospitali kuu ya Muhimbili kwani alihitaji upasuaji wa haraka wa moyo.
Upasuaji ulikamilika sawa lakini hakuamka tena.
Mmoja wa madaktari wa moyo Muhimbili waliomhudumia Marco kwa jina Profesa Haruna Nyagoli ambaye alizungumza kwenye mazishi hayo alielezea kwamba upasuaji ulidumu kwa saa 16.
Kulingana na Nyagoli, upasuaji ulifanikiwa lakini tatizo alilokuwa nalo Marco ni kuvuja damu kwa wingi hali ambayo alisema huwa inatokea baada ya upasuaji na ndiyo ilisababisha kifo chake.
Ameacha mjane na watoto.