Burton Mwemba mtangazaji na mtu maarufu mitandaoni nchini Tanzania anayefahamika sana kama DC Mwijaku ametangaza kwamba Fridah Kajala anarudiana na msanii Harmonize.
Kulingana na video ambayo amechapisha kwenye mitandao ya kijamii, hafla ya kumkaribisha tena Kajala kwenye kampuni ya muziki ya Harmonize Konde Gang inafanyika katika uwanja wa Leaders leo.
Video hiyo inaonyesha watu ambao wanapanga viti na vitu vingine vinavyohitajika kwa hafla hiyo, huku bango kuu likiwa na picha ya Kajala na Harmonize.
Bango hilo limeandikwa maneno “Welcome Back” na Mwijaku anasikika akikaribisha wapenzi wa Konde Gang kwa mkutano huo wa leo.
Harmonize na Kajala waliachana baada ya tetesi kuibuka kwamba alikuwa ananyemelea binti ya Kajala aitwaye Paula.
Tangu wakati huo, Harmonize amekuwa kwenye mahusiano kadhaa ambayo hayadumu na kulingana na Mwijaku ni mapenzi ya Mungu kwamba wawili hao wawe pamoja.
Harmonize hajawahi kumsema vibaya Kajala na kila anapoulizwa huwa anamsifia sana.
Kando na kuwa mpenzi wake, Kajala pia alihudumu kama meneja kwenye kampuni ya Konde Gang lakini usimamizi wake pia ulikumbwa na matatizo kwani wasanii walijitoa wakidai kunyanyaswa.
Inasubiriwa kuona kama kweli anarejea kwenye kampuni hiyo ambayo kwa sasa ina msanii mmoja Ibraah kando na Harmonize.
Wasanii Country Wizzy, Anjella, Killy na Cheedy waliondoka humo.