Msemaji wa serikali Isaac Mwaura, amesema watu 10 zaidi wamefariki kutokana na mvua kubwa inayonyesha hapa nchini katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufikisha idadi jumla ya waliofariki kutokana na mvua hiyo 179.
Kulingana na Mwaura, idadi hiyo inajumuisha watu 164 wazima na watoto 15.
Mwaura alisema watu 20 zaidi wameripotiwa kutoweka katika kipindi hicho, na kufikisha idadi jumla ya waliotokewa kutokana na mafuriko hapa nchini 90.
Aidha takwimu za Mwaura zinaashiria kuwa mafuriko hayo yamesababisha majeraha kwa watu 125, ambao wanapokea matibabu katika vituo mbali mbali vya afya kote nchini.
Msemaji huyo wa serikali, alidokeza kuwa familia 1,127 zimehamishwa makwao na kufikisha 31,341 idadi jumla ya familia zilizohamishwa kutokana na mafuriko kote nchini.
Aliwataka wakenya kuwa makini na kutii maagizo ya kiusalama yanayotolewa na asasi mbali mbali.