Serikali imesema mvua zaidi itanyesha katika maeneo kadhaa hapa nchini hadi tarehe 23 mwezi huu.
Vile vile serikali imewahimiza Wakenya, hasa walio katika sehemu za mashariki mwa nchi na eneo la Pwani kuwa waangalifu zaidi.
Hatibu wa serikali, Issac Mwaura, amesema wakazi wa kaunti za Tana River, Lamu na Kilifi wataathiriwa na mafuriko ya ghafla, maporomoko ya ardhi na kuharibika kwa barabara.
Mwaura alisema serikali imechukua hatua mbali mbali zikiwemo kutoa helikopta na dawa za kuwasaidia wakazi wa kaunti za Garissa na Mandera walioathiriwa na mafuriko.
Mwaura aliyekuwa akiongea na wanahabari katika kituo cha kupanga oparesheni za shirika la msalaba mwekundu jijini Nairobi, alikuwa ameandamana na balozi wa Marekani Meg Whitman ambaye alisema marekani itatoa msaada wa zaidi ya shillingi millioni 150 kuisaidia Kenya kununua chakula.
Mwaura aliongeza kusema nchi hii imenakili vifo sita zaidi kutokana na mvua ya El Nino katika muda wa siku tatu zilizopita.
Mwaura amesema kufikia sasa zaidi ya kambi 170 zimeanzishwa kuwasaidia zaidi ya watu elfu 500 ambao wameathiriwa na mvua ya el nino kote nchini.