Serikali imekariri kuwa Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja anatekeleza majukumu yake bila kuegemea upande wowote, kufuatia hisia zilizoibuliwa kuhusu uwepo wake katika ziara ya maendeleo ya Rais William Ruto katika kaunti ya Nyeri.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura, alifafanua kuwa majukumu ya Inspekta huyo Jenerali wa polisi yanaambatana na wajibu wake, kuhakikisha ushirikishwaji shwari wa usalama chini ya sheria za Huduma ya Taifa ya polisi za mwaka 2011.
“Uwepo wa Inspekta Jenerali wa polisi Nyeri, ni kuambatana na majumu yake. Matamshi yake yaliwiana na ziara ya Rais Ruto bila kutaja chama chochote cha kisiasa au siasa za ushindani,” alisema Mwaura.
Hatibu huyo wa serikali aliongeza kuwa tangu mwezi Machi mwaka 2025, Kanja amekuwa akiongoza operesheni za usalama katika kaunti za Baringo, Samburu, Kirinyaga, Nyeri, Laikipia na Meru.
Mwaura alitoa wito kwa wananchi kupuuzilia mbali madai kwamba uwepo wa Inspekta Jenerali wa Polisi katika mkutano wa Nyeri, ulikuwa na malengo ya kisiasa.
“Serikali imejitolea kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi. Ziara ya Rais sio kampeni za kisiasa,” aliongeza Mwaura.
Aidha alisema asasi za usalama, zitaendelea kutekeleza majukumu ya kuhakikisha usalama katika hafla zote rasmi za serikali, kuambatana na sheria za kimataifa zilizopo.