Mwakilishi wadi mteule katika bunge la kaunti ya Meru ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge hilo Zipporah Kinya ameondoa hoja aliyokuwa amewasilisha bungeni ya mjadala wa kumwondoa mamlakani Gavana Kawira Mwangaza.
Hili ni jaribio la tatu la kumwondoa mamlakani Gavana Mwangaza.
Kinya katika hoja yake aliyowasilisha Jumatano Julai 17, 2024 bungeni alitaja makosa matatu yaliyochochea hatua yake ambayo ni ukiukaji wa katiba, ukiukaji wa sheria za serikali kuu na ile ya kaunti na matumizi mabata ya mamlaka.
Aliongeza kusema kwamba wakazi wa kaunti ya Meru walikuwa wamewasilisha malalamishi kwa wawakilishi wadi kuhusu kile walichokitaja kuwa ukiukaji wa sheria na matumizi mabaya ya mamlaka kwa upande wa Gavana Mwangaza.
Mteule huyo wa chama cha UDA alielezea kwamba walijaribu kusuluhisha masuala hayo yaliyoibuliwa na wakazi bila mafanikio ndiposa akaafikia hatua hiyo ya kuwasilisha hoja ya mjadala wa kumwondoa afisini Mwangaza.
Kinya awali alishauriwa na chama cha UDA aondoe hoja hiyo bungeni isijulikane iwapo ushauri huo ndio ulichochea hatua yake ya leo. Hata hivyo gavana Mwangaza alikimbilia mahakama ambayo ilisimamisha mjadala huo.
Mwangaza ameondolewa mamlakani mara mbili na wabunge wa bunge la kaunti ya Meru na kuokolewa na bunge la seneti ambalo lilitupilia mbali makosa dhidi yake.
Aliondolewa mara ya kwanza Disemba 2022 miezi mitatu tu baada ya kuingia mamlakani na Oktoba 2023.