Mwandaaji na mwelekezi maarufu wa filamu nchini Nigeria Kayode Adewumi Peters amefariki jijini Toronto nchini Canada kufuatia maradhi yaliyomsibu kwa muda mrefu.
Familia ya mwendazake ndiyo ilitoa taarifa za kifo hicho kilichotokea Jumamosi asubuhi kulingana na saa za nchi hiyo.
“Tunasikitika kutangaza kifo cha mpendwa wetu Kayode Peters Adewumi, ambaye aliaga kwa amani asubuhi ya leo Juni 28, 2025, jijini Toronto, nchini Canada” ilisema taarifa hiyo ya familia.
Bila kufichua maradhi yaliyokuwa yakimsibu, familia hiyo ilielezea kwamba alipambana na maradhi hayo kwa ujasiri hadi alipofikia mwisho wa maisha yake.
Kando na talanta yake ya uandalizi na uelekezi wa filamu ambayo iligusa wengi, familia hiyo imemtaja mwendazake kuwa mtu mnyenyekevu, mwema na aliyejitolea kusaidia kila mmoja.
“Aligusa maisha ya wengi, katika tasnia ya filamu na kwingineko na tutamkosa sana” ilimalizia taarifa hiyo.
Wengi wanamfahami Kayode Peters kutokana na kazi yake ya vichekesho ya “Flatmates” ya mwaka 2004 na nyingine iliyokuwa mwendelezo wake iitwayo “My Flatmates”
Aliingilia sanaa akiwa katika chuo kikuu cha Lagos katika kundi la Theatre 15 kabla ya kuingilia maandalizi ya vipindi vya runinga kama Twilight Zone na Papa Ajasco and Company.
Kayode alihusika katika maandalizi ya filamu pendwa kama 13 Letters ya mwaka 2019 na Crazy Grannies ya mwaka 2021 kati ya nyingine.
