Mwanawe El Chapo akanusha mashtaka ya ulanguzi

Marion Bosire
2 Min Read
Ovidio Guzman

Ovidio Guzman, mtoto wa mlanguzi sugu wa dawa za kulevya wa asili ya Mexico Joaquin Guzman almaarufu El Chapo, amekanusha mashtaka dhidi yake katika mahakama moja nchini Marekani.

Makosa yake yanajumuisha ulanguzi na kujipatia pesa kwa njia isiyo halali.

Ovidio alifikishwa mahakamani huko Chicago Jumatatu siku chache baada ya kusafirishwa kutoka Mexico.

Katika kikao hicho cha mahakama kilichokuwa chini ya ulinzi mkali, Ovidio alikuwa amevaa mavazi ya wafungwa ya rangi ya chungwa na miguu yake ilikuwa imefungwa.

Alisaidiwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea mahakamani na mkalimani wa lugha ya Spanish na ulipofika wakati wake akakanusha mashtaka dhidi yake.

Ovidio ambaye anajulikana pia kama El Raton au panya, analaumiwa kwa kushirikiana na wengine kusafirisha dawa za kulevya ambazo ni cocaine, fentanyl, heroin, methamphetamine na marijuana hadi nchini Marekani kinyume cha sheria.

Babake alisafirishwa kutoka Mexico hadi Marekani kushtakiwa mwaka 2017 na akahukumiwa miaka miwili baadaye.

Anatumikia kifungo cha maisha gerezani kwa ulanguzi wa dawa za kulevya na mauaji.

Marekani inaamini kwamba wana wa kiume wanne wa El Chapo ambao kwa pamoja hujiita “The Chapitos” au “The Little Chapos” walirithi usimamizi wa kundi lake la Sinaloa Cartel baada yake kuhukumiwa.

Wanawe wengine watatu nao wamesafirishwa hadi Marekani kushtakiwa.

Wanachama wa kundi lao walichoma magari na kuzua vurugu wakati alitiwa mbaroni mwaka 2019 lakini akaachiliwa haraka kuzuia vifo.

Ovidio ameshtakiwa kwa jumla ya makosa sita na mawili yana adhabu ya lazima ya kifungo cha maisha gerezani.

Marekani ilikubali kwamba haitaangazia kamwe adhabu ya kifo kama sehemu ya makubaliano ya kumsafirisha hadi Marekani ili ashtakiwe.

Atasalia kizuizini hadi siku atahukumiwa. Kesi yake itasikilizwa tena mwezi Novemba mwaka huu.

Share This Article