Bunge la Seneti katika jimbo la Texas nchini Marekani limemwondolea mashtaka ya ufisadi mwanasheria mkuu wa jimbo hilo katika kikao cha kihistoria cha kutafuta kumwondoa afisini.
Matokeo ya kikao hicho cha Jumamosi Septemba 16, 2023 yanatoa fursa kwa Ken Paxton kurejea kazini miezi mitatu baada ya kuondolewa na wanachama wenzake wa Republican kwa kile walichokitaja kuwa matumizi mabaya ya mamlaka.
Paxton, rafiki wa aliyekuwa Rais Donald Trump, alisifia bunge hilo la Seneti kwa uamuzi wa huo akisema ukweli ulishinda.
Alisema katika taarifa kwamba ukweli haungefichwa kabisa na wanasiasa wenye nia ya kumchafulia jina au wadhamini wao wenye uwezo mkubwa.
Trump naye alifurahishwa na uamuzi huo akimpongeza Paxton kwa ushindi wa kipekee na wa kihistoria katika jimbo la Texas.
Paxton ambaye wengi nchini Marekani wamemfahamu kama kikwazo katika serikali ya sasa ya Rais Joe Biden wa chama cha Democrat, ambaye amewahi kuanzisha kesi nyingi za kuzuia utekelezaji wa sera za serikali ya kitaifa alikuwa anakabiliwa ma mashtaka 16.
Kesi dhidi yake katika bunge la Seneti ilianza Septemba 5 ambapo mashahidi walielezea njia zake za kifisadi kwa kina kama kutumia mamlaka yake kumlinda Nate Paul, mkwasi wa sekta ya ujenzi ambaye hutoa michango ya kusaidia wanasiasa wakati alikuwa akikabiliwa na mashtaka.
Inasemekana Paul alilipa wema wa Paxton kwa kumsaidia kuendeleza uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na kulipia ukarabati wa nyumba yake.
Thuluthi mbili ya maseneta 31 wa texas walihitajika kupiga kura ya kukubaliana na kila shtaka dhidi yake lakini hakuna shtaka hata moja liliungwa mkono na zaidi ya maseneta 14, kiwango hitajika kilikuwa maseneta 21.
Mke wake Angela Paxton, naye ni seneta lakini hakukubaliwa kupiga kura kwenye kesi hiyo.