Mwanamuziki wa Zambia Wesley Chibambo, maarufu kama Dandy Crazy ameaga dunia. Haya ni kulingana na tangazo la Rais wa nchi hiyo Hakainde Hichilema kwenye mitandao ya kijamii.
“Kwa huzuni na majonzi mengi tumepokea habari za kifo cha Wesley Chibambo, ambaye wengi wanamfahamu kama Dandy Crazy.” aliandika kiongozi huyo huku akitoa rambirambi zake kwa familia yake na wote waliopenda sanaa yake.
Rais Hichilema alisifia muziki wa Dandy akisema uligusa wengi na kuwaleta pamoja. Alikumbuka pia watu wengine wanne ambao waliangamia kwenye ajali aliyohusika Dandy na kutakia familia zao faraja.
Awali, Rais Hichilema alikuwa amechapisha taarifa nyingine ya kufahamisha umma kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amelazwa hospitalini akiwa hali mahututi baada ya kuhusika kwenye ajali.
Alikuwa ameomba raia wote wa Zambia wamwombee ili aweze kupata nafuu lakini kwa bahati mbaya ameaga dunia.
Dandy Crazy alizaliwa na kulelewa katika mkoa wa Copperbelt nchini Zambia na amekuwa kwenye ulingo wa muziki kwa miongo kadhaa.
Wimbo wake ‘Don’t Kubeba’ ulisikilizwa sana na kujulikana na wengi wakati wa uchaguzi mkuu wa Zambia mwaka 2011. Alikuwa akitumia muziki kuzungumzia mambo yanayohusu jamii na kuwasilisha maoni yake ya kisiasa.
Siku ya mwisho ya mwaka 2024,Dandy Crazy alihusika kwenye ajali katika barabara ya Great North kati ya maeneo ya Kabwe and Kapiri.
Aliachwa na majeraha mabaya ambapo alifanyiwa upasuaji wa dharura katika hospitali ya mafunzo na matibabu maalum ya chuo kikuu cha Zambia.
Tarehe Mosi Januari 2025 kunako saa saba na dakika 42 alfajiri, alikata roho.