Mwanamuziki wa Uganda Mesach Semakula ametangaza mipango ya kufanya harusi na mpenzi wake wa muda mrefu Sarah Nakayi.
Semakula alitangaza hayo kwenye mkutano wa familia uliofanyika kwenye makazi yake uliohudhuriwa pia na marafiki wa karibu na washirika wa tasnia ya muziki.
Mwimbaji huyo amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Sarah tangu mwaka 2002.
Askofu James Bukomeko wa dayosisi ya Mityana ndiye alisababisha Semakula afichue habari za harusi yao kwenye mkutano huo.
Bukomeko alizungumzia suala la harusi hiyo ambayo kulingana naye imechelewa akisisitiza umuhimu wa kuhalalisha ndoa.
“Tunataka kumpa Mesach harusi inayofaa” alisema Askofu huyo huku akimtaka mmoja wa waandalizi wa hafla kwa jina Abitex, aipange kama anavyopanga matamasha ya muziki.
Alisema maandalizi yanafaa kuanza mara moja huku tarehe kamili ya tukio hilo ikitarajiwa kutangazwa mwaka ujao.
Semakula alithibitisha kwamba ana mipango hiyo ya harusi akisema liichelewesha makusudi kutokana na sababu nyingi tu.
Mwanamuziki huyo anaamini kwamba wakati umewadia akifichua kwamba kakake aliunda uwanja mzuri wa ekari tano wa kuandaa hafla hiyo.
“Sasa tuna eneo la tukio. Itakuwa harusi kubwa, itakuwa kama siku kuu ya kitaifa.” alimalizia mwanamuziki huyo.