Mwimbaji wa Thailand Phing Chyada alikwenda kukandwa kama kawaida kufuatia maumivu aliyokuwa akihisi kwenye mabega yake huko Udon Thani, kaskazini mashariki mwa nchi yake.
Wakati wa kukandwa, shingo ilipindwa akapata maumivu ambayo alidhani yatakoma kadri muda ulivyokuwa ukisonga lakini hali ikazidi kuwa mbaya akawa anatumia dawa za maumivu kujituliza.
Wiki moja baadaye, mkono wake wa kulia ukafa ganzi lakini badala ya kwenda hospitalini, mwanamuziki huyo akaamua kwenda kukandwa.
Wiki mbili baada ya hapo maumivu kwenye shingo yakazidi akashindwa hata kulaloa mgongo lakini bado hakuona haja ya kwenda kwa daktari akarejea kwenye chumba cha kukandwa asijue hatari iliyokuwa ikimkodolea macho.
Alipokwenda kukandwa kwa mara ya tatu, taratibu alizopitia zilikuwa za kiwango cha juu ambapo alibaki na michubuko kadhaa. Michubuko ilikwisha lakini dalili tofauti zikajitokeza.
Mwanamuziki huyo alianza kuhisi kama ambaye anachomwa chomwa kwenye ncha za vidole asiweze kutumia kiganja cha mkono wa kulia.
Ganzi hiyo ilisambaa kwenye mkono wake hadi kwenye kifua na mguu wa kulia mpaka ikaathiri upande wote wa kulia wa mwili wake.
Mwanamuziki huyo alisimulia madhila yake kwenye Facebook ambapo alisema nusu ya mwili wake ulikuwa umekufa ganzi.
Siku kadhaa baadaye alifariki na sasa eneo alilokwenda kukandwa linachunguzwa ili kufahamu kilichotokea.